Taka Zangu, Tatizo la Nani? Swali Linaloamsha Dhamiri ya Jamii
Kila siku tunazalisha taka. Baadhi ni chache, nyingine ni nyingi. Tunapomaliza kutumia vitu kama vifungashio vya bidhaa, mara nyingi swali hili halitupi hujirudia kichani: nitaweka wapi hii taka? Badala yake, swali halisi linalopaswa kuulizwa ni hili: nikikitupa hivi, nani ataathirika?
Kwa muda mrefu, jamii imejenga tabia ya kuhamisha lawama. Taka zikiwa mitaani, tunasema ni uzembe wa halmashauri. Zikiziba mitaro, tunalaumu mvua. Lakini kabla ya mvua, kabla ya lori la taka, kulikuwa na mkono wa mtu mmoja mmoja.
Taka Haziibuki Zenyewe
Hakuna taka inayojileta yenyewe barabarani. Kila mfuko wa plastiki, kila chupa, kila mabaki ya chakula, yalishikwa na mtu kabla hayajatupwa. Ukweli huu rahisi mara nyingi huumiza dhamiri, ndiyo maana hujaribiwa kufichwa nyuma ya maneno makubwa kama “mfumo mbovu” au “ukosefu wa mipango”.
Ndiyo, mifumo ni muhimu. Lakini bila maadili, hata mfumo uwe bora kiasi gani lazima utashindwa.
Tatizo la Taka ni Tatizo la Mahusiano
Taka tunapotupa ovyo, hatuyaumizi mazingira tu; tunawaumiza watu, Ebu jaribu kufikia hukusu watu hawa:
- Mtoto anayepata maambukizi kwa kuchezea taka,
- Mama anayepika katikati ya harufu kali ya uchafu kila siku na
- Jamii inayokumbwa na magonjwa yatokanayo na uchafu.
Kama wote tunajua madhara ya utupaji taka ovyo na hatupo tayari kuwajibika, basi yawezekana kila mmoja akawa anasema kimya kimya moyoni "atakayepatwa na madhara atajua mwenyewe, sijukumu langu". Hapo ndipo tatizo linapogeuka kutoka suala la usafi na kuwa tatizo la maadili ya kuishi na wengine.
Kila Mtu Anapowajibika kwa 'nafasi yake', Tatizo Hutoweka
Jamii zinazoogoza kwa usafi duniani, hazijafika hapo kwa sababu zina watu wachache, bali kwa sababu watu wengi wanawajibika kwa walichozalisha na kwa kila wanachotumia. Kila mtu anapobeba dhamana ya taka zake, mzigo wa jamii hupungua.
Lakini pale ambapo kila mtu anafikiri na kusema: “Si yangu”, “Kuna wanaolipwa kufanya usafi”au “Taka moja haitaharibu chochote”. Hapo ndipo taka zinapogeuka kuwa janga la mtaa mpaka taifa kwa ukubwa wake.
Watoto Wanajifunza Kupitia Mfano
Mtoto anapomuona mzazi akitupa taka ovyo, anajifunza bila kufundishwa. Anajifunza kwamba uwajibikaji unaweza kuachwa. Lakini mtoto anapomuona mzazi akibeba taka yake hadi apate sehemu sahihi pa kuitupa, anajifunza somo la maisha: 'kila kitendo kina wajibu wake'.
Hapo ndipo mabadiliko ya kweli huanza, si kwa hotuba, bali kwa vitendo vinavyoonekana.
Je, Taka Zangu Ni Tatizo la Nani?
Swali hili halihitaji jibu la haraka. Linahitaji tafakari. Kwa sababu jibu la kweli mara nyingi ni hili: ni tatizo langu kwanza, kabla halijawa la mtu mwingine.
Jamii yenye afya hujengwa na watu wanaokubali kuwajibika hata pale ambapo wangepata nafasi ya kukwepa. Taka zetu ni mtihani mdogo wa uadilifu wetu wa kila siku.
Hitimisho: Uwajibikaji Unapoanza, Mabadiliko Huonekana
Hatuhitaji mtu wa kutulazimisha. Hatuhitaji adhabu kali kwanza. Tunahitaji dhamiri iliyo hai. Pale ambapo kila mmoja anauliza, “nikitupa taka hii hapa hata kama sijaonekana, je, ni sawa?, je kama sijaoneka bado inaweza kuleta madhara?, na je madhara haya yatakuwa kwangu tu aua yatawagusa hata wasiohusika? kutoka kwenye tafakari ya maswahili haya tunduizi, ndipo jamii huanza kujisafisha yenyewe.
"Taka zangu si tatizo la mtu mwingine. Ni kipimo cha maadili yangu".