Taifa imara linajengwa na vijana imara, vijana imara wanajengwa na jamii imara, ambayo inajengwa chini ya misingi ya maadili imara
Maadili Kwanza ni Taasisi isiyo ya kiserikali yenye lengo la kuishirikisha na jamii na wadau wa maadili katika kufanya tafiti na kuchambua masuala yanayohusu maadili na pamoja na kutoa elimu kwa makundi mbalimbali ya jamii kuhusu kuhusu namna bora ya kuimarisha kueneza na kulinda maadili ya Mtanzania.Taasisi hii itaendeshwa kwa mujibu wa kanuni na taratibu za katiba. Ili kuleta uhalisia na ufanusi katika muongozowake katiba hii itapitiwa na kufanyiwa marekebisho kupitia mkutano mkuu kadri wanachama watakavyoona kuwa inafaa.
Taasisi hii haifungani na upande wowote wa siasa wala dini
Kujenga taifa lenye misingi imara ya maadili, kuanzia kwa mtu mmoja mmoja, familia, jamii hadi taifa kwa ujumla, ambapo vijana wanakuwa viongozi wa kesho wenye uadilifu, uwajibikaji na heshima kwa utu wa binadamu na mazingira.Tunaona Tanzania yenye jamii inayothamini maadili kama chanzo cha amani, maendeleo, mshikamano wa kijamii na ustawi wa vizazi vya sasa na vijavyo.
Ili kufikia maono yetu, Maadili Kwanza Tanzania hutumia mikakati ifuatayo:
Uadilifu ni moyo wa Maadili Kwanza Tanzania. Tunaamini kufanya yaliyo sahihi si kwa sababu ya kutegemea pongezi wala kuepuka kufanya mabaya kwa hofu ya adhabu, bali kwa sababu ni vema kufanya yaliyo sahihi. Tunahimiza maisha ya uaminifu, kusema kweli, na kusimama na haki hata pale ambapo ni rahisi kufanya kinyume chake. Jamii yenye uadilifu hujenga vijana imara, jamii imara na taifa imara.
Tunaamini kila mtu ana wajibu wa kimaadili kwa matendo yake kwa nafsi yake, kwa wengine, kwa mazingira, na kwa vizazi vijavyo. Tunahimiza watu kufikiri kabla ya kutenda, kuelewa athari za maamuzi yao, na kubeba dhamana ya matokeo ya matendo yao. Uwajibikaji huu hujenga jamii yenye nidhamu ya ndani, si jamii inayoongozwa na hofu ya sheria pekee.
Kama Taasisi ya iliyojikita kuyakwamua na kuyaendeleza Maadili, tumeweka kipaumbele kwa ustawi wa jamii dhidi ya maslahi ya mtu binafsi au watu wachache. Ni jukumu letu kuhakikisha kuwa hatua za taasisi yetu zinanufaisha jamii kwa ujumla.
Tunaamini maadili ya kudumu hayawezi kupandikizwa kwa kulazimishwa, bali hujengwa kwa uelewa. Tunakuza utamaduni wa kujifunza, kuuliza maswali, na kufikiri kwa kina kabla ya kuamua. Kupitia tafiti, mijadala na elimu, tunawawezesha watu kuona maadili kama nyenzo ya mafanikio ya maisha, si kikwazo cha maendeleo.
Tunaamini mabadiliko ya maadili hayawezi kufanikiwa bila ushirikiano wa pamoja. Tunafanya kazi kwa karibu na jamii, taasisi, serikali, viongozi wa dini na mila, pamoja na wadau wengine, bila kubagua misingi ya kisiasa, kidini au kikabila. Ushirikiano huu huongeza uhalisia wa suluhisho na kuimarisha umiliki wa mabadiliko ndani ya jamii.
Tunazingatia athari za muda mrefu katika kila tunachokifanya. Tunaamini maadili hayapaswi kutegemea watu binafsi, bali yajengwe kupitia mifumo, elimu na utamaduni unaodumu. Lengo letu ni kuhakikisha kuwa hata tukiondoka, misingi ya maadili itaendelea kuimarika na kulinda ustawi wa taifa kwa vizazi vya sasa na vijavyo
Tunauishi mtazamo wa kuwajibika na kujali mazingira katika shughuli zetu zote. MAADILI KWANZA ni mabalozi wa kulinda na kutunza mazingira. Tunatambua mazingira sio muhimu kwa binadamu tu bali viumbe wote.